DR WILLIBRORD SLAA YU WAPI KISIASA?

Dr Willibrord Slaa

KATIBU Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema anamkubali kwa asilimia 90 mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli akisema anafaa kwa nafasi hiyo kwa kuwa ni jasiri na ana uwezo wa kupambana na ufisadi.

Kutokana na sifa hizo, amesema endapo atakabidhiwa nchi, atasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti rasilimali za nchi na hivyo kuifanya nchi ipae kwa kasi kimaendeleo.

Alisema katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, kuna wagombea urais hawawezi kukemea ufisadi wala kuzungumzia kwa kuwa wao wenyewe sio wasafi, kwa kile alichoeleza ukiwa mchafu huwezi kupata ujasiri wa kumnyooshea mtu mwingine kidole.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha runinga cha Star TV kijulikanacho kama Ajenda 2015 juzi, Dk Slaa aliyejiweka kando baada ya Chadema kupokea makada kutoka CCM wanaodaiwa si waadilifu, alisema kwa sasa anatafutwa Rais wa nchi, lakini mgombea asiyeweza kufafanua sera kwa kushindwa hata kuzungumza kwa dakika 10, hawezi kwenda kuongoza au watakaoongoza ni wasaidizi wake.

Dk Slaa alisema Chadema, chama ambacho awali kilikuwa kinapingana na ufisadi, kwa sasa hakina ajenda hiyo kutokana na kukaribisha wasio wasafi.

Alisema akiwa mpambanaji wa vitendo vya ufisadi, ambavyo vilisababisha kutishiwa kuuawa baada ya kutangaza ‘Orodha ya Mafisadi’ mwaka 2007, sasa anaungana na Dk Magufuli aliyethubutu kusema ataanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi, jambo linaloonesha ana dhamira ya kweli kwa kutaka kutimiza hilo kwa vitendo.

“Ukweli Magufuli ametokana na CCM na ana mapungufu kama binadamu, lakini ukilinganisha kati ya wagombea urais waliopo, yeye ana nafuu na anaonyesha dhamira ya kupigania serikali,” alisema.
Dk Slaa alisisitiza kuwa wakati huu mgombea urais yeyote anahitaji kuwa na wabunge wengi, lakini Magufuli anaonesha dhamira ya wazi kukataa ufisadi kwa kukataa kuwanadi wagombea ubunge wa chama chake, wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo.

Alisema, akiwa Chadema mwaka 2010 walimlaumu Rais Jakaya Kikwete kwa kuwanyanyua mkono wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi, lakini mwaka huu, Dk Magufuli amekataa kufanya hivyo licha ya kuwa ni wagombea kutoka chama chake.

Akizungumzia vitendo vya rushwa na ufisadi, alisema rushwa ndogo zinaathiri wananchi kwa kuwafanya waishi kwa unyonge kuliko kubwa ambazo madhara kwa wananchi wa kawaida ni kidogo. Alisema anasikitika chama chake kilichopata umaarufu kwa ajenda ya rushwa na ufisadi na kusikiliza nyimbo za hamasa kupinga masuala hayo, sasa hawasikiki tena.
“Kwa sasa chama cha ACT ndiyo kimerithi vita ya rushwa na ufisadi na kubeba ajenda kila wanapopita,” alisema.

Alisema Magufuli ameonesha kwa matendo kuwa anayozungumza yanatoka moyoni na siyo mdomoni, kutokana na kutokuogopa kukosa kura za baadhi ya watendaji wanaotuhumiwa kuwa mafisadi.

“Kama anatekeleza leo hajapewa rungu na akipewa itakuwaje, kwani haogopi kupoteza kura kwani ufisadi upo kuanzia vijijini na vitongojini, hatua hiyo ni ujasiri wa ajabu sana kwa mgombea,” alisema.

Alibainisha kuwa kampeni siyo ushabiki wala shamrashamra, bali ni kuangalia viongozi bora kwa kuzingatia sera. Alisema yeye baada ya kusikiliza mikutano na kuangalia kwenye mitandao na kuzingatia mapambano dhidi ya ufisadi, amebaini hakuna mgombea atakayepambana na ufisadi kama Magufuli.

Akizungumzia suala la wagombea wawili wa vyama vya CCM na Chadema kuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi, Slaa alisema kuna michakato inaendelea wakati huu wa kampeni, ikiwemo kupeleka watu katika mikutano na kutoa fedha.

Alisema hali hiyo imefanya iwe vigumu kupima ni nani anakubalika zaidi.
Alisema wapo wananchi wa aina tatu, kwamba wapo wanamjua wanayekwenda kumpigia kura, wengine wanafanya maamuzi kabla ya kampeni na wapo pia wanaofanya maamuzi kwa kubadilika pole pole mpaka mwisho wa kampeni.

Slaa pia alitahadharisha Watanzania kuwa Tanzania ni mama yao, ambaye hawezi kutokea mwingine, hivyo akichezewa, watu wote wataathirika na hawataweza kupata mwingine kama huyo.
Alitaka zifanyike kampeni zinazozingatia amani, kama zilivyofanyika mwaka 2010. Alisema ikiwa itatokea migogoro, hata wanaotangaza uongozi hawawezi kutawala makaburi, hivyo ni vyema kuzingatia misingi ya amani.

Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuzingatia sheria katika kusimamia uchaguzi na kuepuka kuwa sababu ya vurugu. Slaa alisema kamwe Watanzania wasikubali masuala ya kwenda Ikulu, kuleta balaa nchini bali kwa ujumla kuzingatia masuala ya kitaifa.

Previous
Next Post »
Show Comments: OR

Contact us

Name

Email *

Message *

Tangaza nasi

Tangaza nasi
Freebango.com