Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha CCM John Pombe Magufuli ndiye rais mteule wa taifa la Tanzania baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.
Akitoa
matokeo hayo mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Jaji
Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Magufuli alijipatia kura 8,882,935
ikiwa ni aslimia 58.46 huku mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa wa
chama cha Chadema akijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya
kura zote.
Haya ndiyo matokeo kamili kama yalivyotangazwa na Jaji Lubuva:
Matokeo ya uchaguzi wa urais Tanzania | |||
---|---|---|---|
Jina | Chama | Kura | Asilimia |
Anna Mghwira | ACT | 98,763 | 0.65 |
Chifu Yemba | ADC | 66,049 | 0.43 |
John Magufuli | CCM | 8,882,935 | 58.46 |
Edward Lowassa | CHADEMA | 6,072,848 | 39.97 |
Hashim Spunda | CHAUMA | 49,256 | 0.32 |
Janken Kasambala | NRA | 8,028 | 0.05 |
Macmillan Lyimo | TLP | 8,198 | 0.05 |
Fahmi Dovutwa | UPDP | 7,785 | 0.05 |
Awali kabla ya kutolewa kwa matokeo hayo vyama vya siasa
vilivyokubaliana na matokeo vilitia sahihi matokeo hayo. Lakini chama
cha Chadema, chake Bw Lowassa hakikuwakilishwa. Chama hicho kimepinga
matokeo hayo.
Akivihutubia vyombo vya habari mgombea wa urais
kupitia chama hicho Edward Lowassa amepinga matokeo yoyote ya uchaguzi
huo na kujitangaza mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 62 ya kura
zilizopigwa.
Lowassa amedai kwamba tume ya uchaguzi nchini humo
imeshirikiana na chama tawala CCM kufanya udanganyifu katika shughuli
hiyo, madai ambayo tume hiyo imekanusha.
"Hatuna hata chembe ya
wasiwasi kwamba mchakato huu ulifuata sheria na ni halali," alisema Jaji
Lubuva muda mfupi kabla ya kutangaza matokeo.
Aidha, amesema tume iliendesha mchakato wote "bila shinikizo".
Akizungumzia kutoidhinishwa kwa matokeo hayo na wawakilishi wa
Chadema, mkurugenzi wa uchaguzi katika tume Bw Ramadhan Kailima alisema
sheria inawaruhusu kuendelea na kutangaza matokeo hata bila chama
chochote kile kuwakilishwa au kuidhinisha matokeo husika.
Kwenye
uchaguzi huo, kati ya wapiga kura 23,161,440 waliojiandikisha, ni
15,589,639 waliopiga kura, ambao ni asilimia 67.31 ya wapiga kura wote.
Kura 402,248 ziliharibika.
Kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo,
tume hiyo ya uchaguzi sasa inatarajiwa kumkabidhi Bw Magufuli cheti cha
kuwa mshindi wa urais.
Sign up here with your email