CCM inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa wanachama, wapenzi na washabiki wake na kwa umma Watanzania.
Tathmini ya Upigaji Kura
Kama
tulivyoeleza jana, tumeridhishwa na amani na utulivu uliotawala katika
sehemu kubwa ya nchi yetu wakati wa zoezi la upigaji kura. Licha ya
changamoto zilizojitokeza, ambazo baadhi zimeshughulikiwa, kwa jinsi
zoezi la kupiga na kuhesabu kura lilivyoendeshwa kwa uwazi, matokeo ya
uchaguzi huu yatakuwa ni kielelezo cha utashi halisi wa Watanzania na
kutakuwa hakuna sababu ya mtu yoyote kukataa matokeo.
Kupokea na Kutangaza Matokeo
Kipindi cha
kupokea na kutangazwa matokeo ni muhimu kama ilivyo kipindi cha kampeni
na siku ya kupiga kura. CCM inahimiza utulivu kwa wafuasi wake na
wananchi kwa ujumla na kuziachia mamlaka husika zifanye kazi yake.
Katika kipindi hiki, kazi za vyama ni kupokea matokeo na na kazi ya Tume
ni kutangaza matokeo.
Tunasikitishwa
na propaganda zinazoendeshwa na wapinzani wetu kuhusu matokeo ya
uchaguzi. Tunaona matokeo yanayotangazwa na wafuasi wa vyama vya
upinzani, hasa mitandaoni. Bahati nzuri, propaganda hizi zinakosa
maarifa kiasi cha kutoa hata matokeo ya Ubunge katika majimbo ambayo
uchaguzi wa Wabunge haukufanyika, mfano Handeni na Masasi.
Tunawataka
wana-CCM wapuuze matokeo yanayotembezwa kwenye mitandao ya kijamii.
Matokeo rasmi yatatolewa na Tume. Bahati mbaya sana, wenzetu wanatoa
matokeo ya uongo mapema ili Tume ikitoa matokeo rasmi waseme wameibiwa
kura na kutafuta kisingizio cha kuingia mitaani na kufanya vurugu. Pia
tunabaini jitihada na nguvu kubwa za wapinzani wetu kupeleka kilio chao
kwa waandishi wa habari wa nje ya nchi pamoja na mataifa ya nje kwa
ujumla.
Wameajiri magwiji wa propaganda kutoka nje ya nchi kwa fedha
nyingi kujenga taswira kwenye Jumuiya ya Kimataifa kwamba Tanzania ni
kama nchi nyingine yoyote ya Kiafrika ambapo hakuna ustaarabu wala
utaratibu wa kidemokrasia na Serikali hukandamiza watu wake. Mkakati wao
ni kuitaka Jumuiya ya Kimataifa itumie nguvu yake ya misaada kwa nchi
yetu kulazimisha matokeo ambayo hayatokani na utashi wa Watanzania. CCM
haitalikubali jambo hili.
Matokeo ya CCM
Kwa kuwa
matokeo kwenye vituo vya kupigia kura matokeo yamebandikwa hadharani na
Wasimamizi wa Vituo, na nakala kupewa mawakala wetu, kwa mujibu wa
matokeo yaliyobandikwa vituoni , CCM hadi sasa imekwishapata majimbo 176
kati ya majimbo 264 katika mikoa kadhaa ambayo tumefanikiwa kujumlisha
hadi sasa. Pia, hadi sasa, tumeweza kukomboa majimbo 11 ambayo yalikuwa
upinzani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Tunawaomba
wana-CCM watulie, wasiwe na hofu, wawe na subira hadi Tume imalize kazi
yake. Matokeo ya Urais, ambayo yanaendelea kutangazwa na Tume, hayana
tofauti na mwenendo tunaouona katika kura za Ubunge.
Imetolewa:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
26.10.2015
Sign up here with your email