JK Afungua majengo ya Hazina, Benki Kuu tawi la Dodoma na Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete akifungua jengo la hazina ya Benki kuu ya Tanzania tawi la Dodoma
 
RAIS Jakaya Kikwete amesema kumekuwa na nidhamu kwenye matumizi ya fedha za serikali pamoja na kuongezeka kwa mapato yake. Alisema hayo jana mjini hapa wakati akifungua majengo ya Hazina, Benki Kuu tawi la Dodoma na Ofisi ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali.

Rais Kikwete alisema tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mapato ya fedha za serikali yameongezeka. “Kumekuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na ukusanyaji wa mapato umeongezeka,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa miongoni mwa mambo yaliyochangia kuongezeka kwa ufanisi ni pale serikali ilipoajiri wahasibu ngazi ya CPA wapatao 780 kwenye halmashauri za wilaya ambako awali hata uandishi wa vitabu vya hesabu ulikuwa ni tatizo. “Tumefika mahali pazuri, taarifa nzuri na makosa mengi yamerekebishwa,” alisema na kuongeza kuwa pia ofisi nyingi za ukaguzi ziko kwenye majengo ya serikali, jambo linalofanya wakaguzi wasiwe huru kufanya kazi zao.

Alisema ameridhishwa na viwango vya ubora wa majengo yaliyozinduliwa na kutaka kuboreshwa kwa eneo linalozunguka majengo hayo ili yaendelee kuwa na hadhi yake.

Alisema sehemu ya mbele ya majengo kukiwa kuchafu thamani ya majengo inashuka, hivyo itengenezwe bustani ili majengo yawe na thamani. “Nimemwambia Mkuu wa Mkoa hatutegemei kati ya majengo haya wananchi wagawiwe viwanja lazima kupanda miti vizuri kulia na kushoto na viwanja vinavyogawiwa kuwe na viwango vya majengo,” alisema Rais Kikwete.

“Pangeni mji vizuri ili Dodoma ipendeze polepole hii ndio safari ya kujenga makao makuu,” alisema Rais Kikwete na kuagiza kupimwa kwa eneo lote la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ili kusiwe na mji hohela.

Awali, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema ujenzi wa majengo hayo ni utekelezaji wa maagizo ya serikali kujenga na kuendeleza makao makuu ya serikali Dodoma.

Ujenzi ulianza mwaka 2010 kwa ujenzi wa jengo la (BoT), jengo la Hazina na mwaka 2012 ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Previous
Next Post »
Show Comments: OR

Contact us

Name

Email *

Message *

Tangaza nasi

Tangaza nasi
Freebango.com