Mwandishi wa habari kuifikisha serikali Mahakamani


MWANDISHI wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kukuza Utawala Bora na Uwazi, Edwin Soko anatarajia kuipandisha kizimbani serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Soko amewaambia waandishi wa habari kuwa ana nia ya kuifikisha serikali mahakamani chini ya kifungu cha. 6(2) Sheria ya mwenendeo wa makosa sura ya 5 ya sheria za Tanzania juzuu la 2002 , kikisomeka pamoja na kifungu cha. 3,6(b)c.
Serikali inatuhumiwa tuhuma za kutunga kanuni ndogo za utangazaji kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, huku ikijua kuwa inakiuka ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nimewaita hapa kwa ajili ya kuwaambia kuwa, ninafungua kesi ya kikatiba dhidi ya serikali kufuatia kuwepo kwa baadhi ya vifungu ndani ya kanuni ndogo za maudhui ya utangazaji 2015, zinazokiuka katiba ya nchi na kuminya uhuru wa mtu na chombo kupata taarifa na kuzisambaza kwa mujibu wa katiba,” amesema Soko kwenye mkutano huo uliofanyika ofisi za UPTC jijini Mwanza.

Aliongeza kwamba licha ya kubaki siku chache, kimsingi yeye pamoja na wanahabari wengine walihitaji muda wa kujiridhisha kwa kina juu ya uwepo wa vifungu ndani ya kanuni vinavyokiuka haki ya kikatiba kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 18, kazi hiyo ilihitaji muda wa kutosha ili kufanya uchambuzi wa kina na kubaini mapungufu.

Alibainisha baadhi ya vifungu hivyo kuwa ni kanuni ndogo za maudhui ya utangazaji 2015, vinavyokiuka katiba ya nchi baadhi ya vifungu hivyo ni 15(2),6(a) (7) (a) na (b), 8(2), 10 (10)(a), 9(2), (3) sanjali na utangulizi wa sehemu ya tatu ya sheria unaosema hakuna kutangaza siku ya upigaji wa kura, huku kwenye maudhui ya sheria hii inaruhusu matangazo.

Kanuni hizo zilizotangazwa kwenye gazeti la serikali Juni 26, 2015 zinaminya uhuru wa mtu kupata na kutoa taarifa kwa mwananchi na pia haki ya vyombo vya habari vya luninga na redio kupata na kusambaza taarifa, kwani vinawekewa vizingiti visivyokuwa na lazima kisheria.

Athari za kanuni hizo kwa mujibu wa maelezo ya Soko, kuwa wananchi wanapokonywa nguvu ya kikatiba waliyopewa katika ibara ya 18(a),(b),(c) na (d) kwa kutotakiwa kushiriki kwenye programu na pia vyombo vya habari vinanyimwa fursa ya kutafuta na kufikisha taarifa mbalimbali za mwenendo wa uchaguzi kwa wananchi kwa kuwekewa mipaka ya kuripoti wakati wa kampeni na siku ya kupiga kura.

Athari nyingine ni kuwa wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na wanahabari hawapo salama kwa mujibu wa kanuni hizi zenye uwezo wa kuwashughulikia na matokeo yake yakaonekana kwa wananchi kukosa taarifa muhimu.

Soko ameithibitishia MwanaHalisi Online kuwa hatua za awali za ufunguaji wa kesi, ikiwa mosi ni kutoa notisi kwa serikali, hatua hiyo tayari imefanywa na notisi zimesambazwa kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Previous
Next Post »
Show Comments: OR

Contact us

Name

Email *

Message *

Tangaza nasi

Tangaza nasi
Freebango.com