WANANCHI wametakiwa siku ya kupiga kura kuwa macho na watu wanaoweza
kwenda kuwanunua kwa kuwagawia fedha wabadilishe msimamo wao. Mgombea
urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, alitoa hadhari
hiyo jana mjini hapa kwenye mkutano wa kampeni uliohudhuriwa na maelfu
ya watu.
Magufuli ambaye aliendelea kusisitiza kuwa mtu anayenunua watu hawezi
kuona aibu kuuza haki zao, alisema zipo taarifa za wengine wanaonunua
shahada ambao wananchi wanapaswa kuwa macho nao.
“Siku ya kupiga kura, kuna watu wanaweza kupita na kutoa fedha…
ukiona mtu ananunua shahada, anatumia fedha kukununua, hataona aibu
kukuuza, kwa maana ya kuuza haki yako ya maendeleo,” alisema.
Pia katika mkutano wa kampeni aliofanya mjini Kiomboi, Magufuli
alisema, “nimesikia tayari kuna watu wanaanza kupita na kununua shahada
na wengine wanapita wanatoa hela. Hela kuleni lakini kura pigeni kwa
CCM.”
Akiahidi kusimama imara na kulinda maslahi ya Watanzania, alisisitiza
namna ambavyo kwenye mchakato wa kampeni kwenye kura za maoni, hakuna
aliyekula fedha yake. Katika hatua nyingine, Mkoa wa Singida umeahidiwa
neema ya kujengewa hospitali itakayohudumia mikoa ya Kanda ya Kati na
mingine iliyo jirani ambayo itakuwa kubwa kama ilivyo Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili.
Aidha Dk Magufuli, ameahidi mkoa huo utapata uwanja mkubwa wa ndege
utakaopanua wigo wa usafiri kwenda mkoani humo. “Nataka hospitali ya
Kanda itakayojengwa Singida iwe kubwa kama Muhimbili.
Mikoa yote ya jirani wafike kutibiwa hapo.” Alimpongeza Mkuu wa Mkoa
Singida, Dk Parseko Kone kwa kusimamia mchakato huo kuhakikisha
hospitali hiyo inajengwa. Wakati huo huo Magufuli alimpongeza aliyekuwa
Mbunge wa Singida Mjini, Mohamed Dewji na akisema anapenda wawekezaji
wazalendo wanaoipenda Tanzania.
Alimuahidi kumpa ushirikiano atakapohitaji kuwekeza. “Na wewe kama
unapenda kujenga kiwanda chochote nitakuunga mkono…,” alisema Magufuli.
Alimuomba atengeneze hata viwanda vitatu awezeshe wananchi wa Singida
wapate ajira.
Nitakuunga mkono kwa asilimia 100 kama ni kibali unataka, nitakupa
leo hii hii kwa kuwa mmenihakikishia nitakuwa rais,” alisema. Alisema
mji wa Singida ni wa kibiashara hivyo atahakikisha unakuwa na lami
kwenye barabara za ndani.
Kuhusu uwanja wa ndege, alisema utawezesha wawekezaji wanaotaka kuja
kwa ajili ya biashara, wapate fursa ya kutumia usafiri wa anga.
Source: Habarileo
Sign up here with your email
