MAGUFULI: Ahidi kukuza ukuaji wa Uchumi Kirimanjaro


MGOMBEA urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli, jana aliuteka mji wa Moshi mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kuvuta umati mkubwa wa watu aliowakuna kwa hotuba yake iliyosheheni ahadi nzito, zikiwamo za kuondoa kero zinazowakabili na pia kuahidi kupaisha uchumi wa mkoa kwa ujumla.

Katika mkutano wake wa kampeni mjini hapa, Magufuli alisema endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano baadaye mwezi huu, atahakikisha Moshi inapaa kiuchumi. Ameahidi atashughulikia ukubwa wa ushuru, kutolipwa vizuri kwa wabeba mizigo katika Mlima Kilimanjaro, kushuka kwa utalii na kusema ana `dawa’ ya kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni mbili mjini Moshi.

Katika hotuba yake iliyokatishwa mara kwa mara kwa makofi, nderemo, hoihoi na vifijo kutoka kwa wakazi wa mji huo, ambao kwa zaidi ya muongo mmoja unaongozwa na chama cha upinzani cha Chadema, alitaka sasa wakipumzishe chama hicho kwa kuwa kimeonekana kushindwa kuwapa wanaMoshi maendeleo. Mbali ya kupania kupaisha utalii, alisema atarudisha viwanda katika mji huo, huku akiwatengenezea wafanyabiashara mazingira bora ya kufanya shughuli zao.

Alisema endapo atakuwa Rais, atahakikisha wafanyabiashara wa soko la mitumba la Memorial hawahamishwi. “Bado siku 17, kwa kuwa wingi wenu unaonesha mtanipa urais, niwahakikishie mtarajie mambo mazuri kutoka Serikali ya Magufuli,” alisema na kusisitiza kama kuna mnunuzi anayeshindwa kufufua kiwanda, ajiandae kupokonywa kwani huyo anakwamisha ajira na maendeleo ya wakazi wa mkoa huo.

Alitumia pia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Moshi, Davis Mosha akisema ni kijana mchapakazi na mwenye kiu ya kuweka historia ya kuwapelekea wakazi wa Moshi maendeleo endelevu.

Awali, akiwa Bomang’ombe wilayani Hai, Dk Magufuli alisema pamoja na urafiki wake na Mbowe, lakini uwezo wake katika kuwaletea maendeleo wakazi wa Hai akiwa Mbunge ni mdogo na kuwataka wakazi wa jimbo hilo kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Dunstan Mallya.

Alisema pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Hai kuwa chini ya Chadema, kero za wananchi ikiwemo maji, barabara na nyinginezo haziridhishi na badala yake Mbowe amekuwa akisafiri Ulaya, kuzungukazunguka katika majimbo mengine na kushabikia mambo yasiyo na msingi kwa wakazi wa Jimbo la Hai.

Alishangazwa na hatua ya kutofanya kazi kwa Kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools kilichopo wilayani Hai na kuua ajira kwa wakazi hao, huku Mbowe akiwa kimya bila kuwasemea wananchi juu ya kitendo hicho hatua aliyosema inatia shaka uhusiano wake na mmiliki wa kiwanda hicho wa sasa.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema Dk Magufuli ni chaguo la Mungu. Alisema hilo linadhihirishwa na hatua ya mgombea huyo, kutotumia fedha katika harakati zake za kuwania kuteuliwa na chama hicho kuwa mgombea urais, lakini pia kwa wananchi kumuunga mkono kwa nguvu tangu alipoanza kampeni za urais.

Aidha, Dk Nchimbi alieleza pia kukerwa na uzushi kwamba yupo mbioni kujiunga na Umoja wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa na kusema uzushi huo ni ndoto ya mchana na kamwe hawezi kufanya hivyo kutokana na upinzani kuwa katika hatua za kufa.

“Mimi kuhamia Ukawa ni ndoto ya mchana, haiwezekani mtu akashuka kwenye basi la luxury (starehe) akahamia kwenye basi bovu ambalo halijatembea kwa miaka zaidi ya 10. Upinzani umeelemewa na huu uzushi kwangu unanikera na utawasababishia kipigo kikali Oktoba 25,” alisema.

Dk Magufuli na Dk Nchimbi waliyasema hayo kwa wakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara, iliyofanyika kwa siku nzima jana na kuhitimishwa na mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Dk John Magufuli uwanja wa Mashujaa mjini Moshi.

Chanzo: Habarileo
Previous
Next Post »
Show Comments: OR

Contact us

Name

Email *

Message *

Tangaza nasi

Tangaza nasi
Freebango.com