POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inawashikilia watu saba,
wakiwemo sita wa familia moja kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya
ugaidi. Kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni muendelezo wa operesheni
inayoendeshwa na Polisi Kanda hiyo pamoja na mikoa jirani ya kuwatafuta
watuhumiwa wote waliojihusisha na matukio ya kupanga kuvamia vituo vya
polisi, kuua askari na raia na kupora silaha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisi kwake, Kamanda wa kanda
hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema watuhumiwa hao sita ni wa familia
ya mtuhumiwa aliyetajwa kama kiongozi wa kundi linalojihusisha na
vitendo hivyo Ally Ulatule.
“Hawa watu sita ni miongoni mwa familia ya Ulatule na inaonekana
wanahusika moja kwa moja na vitendo hivi, lakini jeshi la polisi
tunaendelea na operesheni ya kuwatafuta wote waliohusika,” alisema Kova.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Mohamed Ulatule maarufu kama
uso wa Simba (67), Hamis Ulatule (51), Ally Ulatule (65), Nassoro
Ulatule (83) wote wakazi wa Mamdimkongo, Mkuranga mkoani Pwani, Said
Chambeta maarufu kama Mzee wa Fasta (40) muuza mitumba mkazi wa Yombo
Makangarawe na Ramadhani Ngande (29) dereva bodaboda mkazi wa Kongowe.
Watuhumiwa hao wanafanya idadi ya watu waliokamatwa kwa tuhuma za
kujihusisha na ugaidi kufikia 7. Katika hatua nyingine, Kova alisema,
wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa waliojihusisha na mauaji ya Ofisa wa
Polisi Elibariki Palangyo yaliyotokea Agosti 4, mwaka huu nyumbani kwake
Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo alisema, kiongozi wa kundi hilo aliyemtaja kwa jina la
Said Mazinge maarufu kama Omary Salehe au Bonge Mzito (39) alipigwa
risasi na kujeruhiwa baada ya kujaribu kuwatoroka askari kwa kujirusha
kutoka kwenye gari.
Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Rashid Watson maarufu kama Dodo
(21), Ramadhani Salum maarufu kama Nguzo (38), Bakari Rashid (38) na
Hamis Hamis maarufu kama Freemason (24).
Alisema mtuhumiwa Watson alikamatwa maeneo ya Vingunguti akiwa na
silaha aina ya Shotgun iliyokatwa mtutu na kutengenezwa kienyeji ikiwa
na risasi nne na betri mbili zilizounganishwa kwa ajili ya kulipua
baruti. Aidha alisema, wamekamata bunduki aina ya SMG moja, shotgun mbili,
bastola moja pamoja na risasi 14. Aidha, alisema Polisi wamefanikiwa
kuokoa mali yenye thamani ya Sh milioni 159.
Chanzo: Habarileo
Sign up here with your email