Kada
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Moshi Vijijini aliyefahamika kwa
jina moja la Kizito, amenusurika kuuawa na wananchi wenye hasira katika
kijiji cha Uru Mawela, baada ya kukamatwa akiwa na makaratasi yenye kura
za mfano za wagombea wa ubunge na udiwani wa jimbo hilo.
Kizito
aliyekuwa akitumia gari dogo aina ya Toyota Verosa lenye namba za
usajili T 756 CPB, alikumbwa na mkasa huo jana saa 10:00 jioni wakati
akitokea katika kituo cha kupigia kura cha Uru-Mawela. Katika tukio
hilo, wananchi hao wanadaiwa kumjeruhi vibaya kada huyo na kisha
kuliharibu gari lake kwa kuiba matairi yote manne, vifaa mbalimbali
ikiwamo pia kadi ya usajili wa gari hilo.
Inadaiwa
kuwa wananchi wa kijiji cha Uru-Mawela walimtilia shaka kada huyo na
kuanza kumfuatilia tangu majira ya mchana na ilipofika saa 10 kasoro za
jioni, walimvamia akiwa barabarani na kulifanyia upekuzi ambapo
walimkuta akiwa na bahasha mbili zenye karatasi hizo ambazo hata hivyo,
zilielezwa kuwa siyo karatasi halisi za kupigia kura.
Paparazi
ilishuhudia kada huyo akiwa chini ya ulinzi wa magari mawili ya askari
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliowahi kufika eneo hilo na
kumuokoa asiendelee kushambuliwa na wananchi hao na gari lake
lisiteketezwe kwa moto.
Kamanda
wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, alithibitisha kutokea
kwa tukio hilo na kueleza kwamba kada huyo baada ya kuokolewa alipelekwa
Kituo Kikuu cha Polisi Moshi Mjini kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na
tukio hilo.
“Wananchi
hao wenye hasira kali, wameliharibu vibaya gari la kada huyo na kuiba
matairi yote, vifaa mbalimbali na kisha kulitelekeza likiwa limechakaa.
Hata hivyo, huyo kada wa CCM tumemchukua na kumpeleka Kituo Kikuu cha
Polisi Moshi Mjini kwa ajili ya kumhoji na baadaye tuanze operesheni za
kuwasaka waliohusika katika tukio hilo,” alisema Kamanda Ngonyani.
Mgombea
ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Dk. Cyril Chami, anachuana
vikali na mpinzani wake wa siku nyingi Anthony Komu, ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) taifa.
Sign up here with your email