WAKAZI wa kata za Makuyuni na Kilema Kati wilayani Moshi Vijijini
wamekamata baadhi ya masanduku na vifaa vya kupigia kura katika Jimbo la
Vunjo juzi vinavyodaiwa kuwa ni kwa ajili ya kusaidia ushindi kwa
baadhi ya wagombea.
Hata hivyo, baadaye ilielezwa kwamba vifaa hivyo ni halali. wakihojiwa Julius Materu na Alex Franklin walisema
vifaa hivyo kukutwa mitaani katika kata hizo usiku ni maandalizi ya
vyama kupata ushindi wa batili.
“Haiwezekani vifaa vya kura visafirishwe usiku tena bila ulinzi wa
Polisi. Tunataka jambo hili lichunguzwe kikamilifu,” alisema Materu. Kwa
upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani
alithibitisha kukamatwa kwa masanduku na vifaa vingine vya kupiga kura
katika kata za Makuyuni na Kilema Kati na kwamba hapakuwa na ulinzi wa
Polisi jambo ambalo pia limelitia shaka jeshi lake.
Alisema watu waliokamatwa na vifaa hivyo ni watumishi wa halmashauri
na kwamba walikamatwa saa 4.15 usiku, hali iliyozua taharuki kiasi cha
wananchi kuzunguka Kituo cha Polisi Himo.
“Ni kweli walikamatwa watu wawili wakiwa na vifaa vya kupigia kura,
hata sisi tuliingiwa na wasiwasi kwamba kwanini hawakuwa na ulinzi wa
Polisi, lakini tulipowahoji walidai ni watumishi wa halmashauri ndipo
ilipoamuliwa vifaa vile vihifadhiwe Kituo cha Polisi Himo kwa usalama
zaidi,” alisema.
Ngonyani alisema baada ya hali hiyo kutokea, Polisi ilimtaka
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Fulgence Mponji
ambaye aliwatambua watumishi hao na kusema kwamba vifaa hivyo ni halali
na siyo vinginevyo.
Hata hivyo, vifaa hivyo vilisambazwa jana asubuhi kwa ajili ya
kupigia kura ingawa Jeshi la Polisi kupitia maofisa wake wakiwamo wa
mkoa wanafanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na hasa ni kwa nini
polisi hawakuwepo kwenye gari lililokuwa na vifaa hivyo.
Sign up here with your email