Wananchi wa Kata ya Embaseni wilaya ya Meru jana walifanya fujo na
kutaka kuchoma gari la Utalii ambalo limekodishwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kwa Halmashauri ya wilaya ya Meru kwa madai ya kuwa
lilibeba kura hewa na kutaka kuziingiza vituoni.
Hali hiyo imetokea jana katika kata hiyo majira ya saa 3:30 asubuhi
hadi saa 4:00 asubuhi mara baada ya vijana kulisimamisha gari hilo kwa
muda na kudai kuwa limebeba kura hewa na kutaka kulichoma moto.
Mara baada ya wasimamizi wa NEC waliokuwa ndani ya gari hilo
kuwaeleza vijana hao kuwa gari hilo halina kura hewa bali lina fedha za
kuwalipa wasimamizi wa uchaguzi na kila kata magari hayo yapo lakini
halina kura hewa.
“Hakuna kura hewa na wala hatuna mpango wa kuiba kura bali hili gari
limebeba fedha za kuwalipa wasimamizi wa uchaguzi na kama mnataka
tuwaonyeshe majina yao ili mthibitishe na kiwango cha fedha
wanachostahili kulipwa,” alisema.
Mara baada ya purukushani hiyo askari waliokuwepo eneo la tukio
waliwaamuru vijana hao kuondoka na kwa wale wanaosubiri kupiga kura
wapige kura kwani hakuna kura yoyote iliyobebwa ndani ya gari hilo.
Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya , Jimbo la Arumeru Mashariki, Damari
Mchome alisema kuwa si kweli kama watu wanavyodai kuwa gari hilo
lilibeba kura hewa bali ukweli ni kuwa gari hilo lilibeba fedha kwa
ajili kuwalipa wasimamizi wa NEC waliochaguliwa na halmashauri hiyo.
Alisema pia halmashauri hiyo imekodisha magari 26 kutoka kampuni
mbalimbali za utalii kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi wa NEC kwani
halmashauri hiyo ina magari matano tu ambayo hayatoshelezi kutoa huduma
kwa Jimbo la Arumeru Mashariki.
Mchome alisema ndani ya gari hilo kulikuwa na mhasibu pamoja na
msimamizi wa uchaguzi msaidizi pamoja na orodha ya malipo kwa wasimamizi
wa NEC na gari hilo ambalo hakulitaja namba zake kuwa lilikuwa na kiasi
cha zaidi ya Sh milioni sita ambazo baada ya tafrani hiyo fedha zipo
salama na hakuna kura yoyote itakayoibwa.
Halmashauri hiyo ina jumla ya wapiga kura 160,647 na vituo vya wapiga
kura vikiwa ni 437 na kata 26. Hata hivyo wananchi wa Jimbo la Arusha
Mjini wanamchagua Rais na madiwani kutokana na Mgombea Ubunge wa
ACT-Wazalendo Estomih Mallah kufariki dunia.
Chanzo: Habari leo
Sign up here with your email