Mchungaji Christopher Mtikila (1950 - 2015)
Mwanasiasa mashuhuri nchini na Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amefariki dunia na watu wengine watatu kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa kilichopo Chalinze mkoani Pwani alfajiri ya leo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed, amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa "Taarifa za mwanzo" zinasema
Mtikila amefariki majira ya saa 11:45 alfajiri ya leo katika kijiji cha
Msolwa, Chalinze.
Amesema gari alilokuwa amepanda Mtikila lilikuwa linatoka mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam, ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wanne ambapo wengine watatu wamejeruhiwa vibaya na kupelekwa katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha, Pwani kwa matibabu.
Wasifu wa Mchungaji Mtikila:
Mtikila alizaliwa mkoani Iringa mwaka 1950. Pamoja na shughuli za
siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa Kanisa la
Kipentekoste la Full Salvation Church.
Enzi za uhai wake Mchungaji Mtikila alikuwa akijihusisha pia na
harakati za haki za binadamu kupitia kitengo cha haki za binadamu cha
kanisa hilo kiitwacho Liberty Desk.
Maisha yake katika siasa:
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Mchungaji Mtikila alijipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu uhujumu wa uchumi uliokuwa unafanywa na wahindi (ambao aliwaita Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za Tanzania.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Mchungaji Mtikila alijipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu uhujumu wa uchumi uliokuwa unafanywa na wahindi (ambao aliwaita Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za Tanzania.
Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar. Alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na siyo
Tanzania. Hata hivyo Mtikila alibadili msimamo wake katika miaka ya
karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama kutoka Zanzibar (kama sheria ya
uchaguzi inayotaka) na hivyo chama chake kuweza kupata usajili wa
kudumu.
Mtikila alikuwa ni kati ya wagombea 10 wa nafasi ya urais katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Katika uchaguzi huo alipata asilimia 0.27
ya kura zote.
Kesi na kifungo:
Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja kesi ya kutaka
wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa
Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya
siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali kutoka kwa mkuu wa
wilaya na polisi.
Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na
hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM,
marehemu Horace Kolimba.
Mwaka 2004 alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa
kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. AMEN
Chanzo:Global Publishers
Sign up here with your email