Dr Willibrord Slaa
KATIBU Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema
anamkubali kwa asilimia 90 mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John
Magufuli akisema anafaa kwa nafasi hiyo kwa kuwa ni jasiri na ana uwezo
wa kupambana na ufisadi.
Kutokana na sifa hizo, amesema endapo atakabidhiwa nchi, atasaidia
kwa kiasi kikubwa kudhibiti rasilimali za nchi na hivyo kuifanya nchi
ipae kwa kasi kimaendeleo.
Alisema katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa
Oktoba 25, kuna wagombea urais hawawezi kukemea ufisadi wala kuzungumzia
kwa kuwa wao wenyewe sio wasafi, kwa kile alichoeleza ukiwa mchafu
huwezi kupata ujasiri wa kumnyooshea mtu mwingine kidole.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha runinga cha Star TV
kijulikanacho kama Ajenda 2015 juzi, Dk Slaa aliyejiweka kando baada ya
Chadema kupokea makada kutoka CCM wanaodaiwa si waadilifu, alisema kwa
sasa anatafutwa Rais wa nchi, lakini mgombea asiyeweza kufafanua sera
kwa kushindwa hata kuzungumza kwa dakika 10, hawezi kwenda kuongoza au
watakaoongoza ni wasaidizi wake.
Dk Slaa alisema Chadema, chama ambacho awali kilikuwa kinapingana na
ufisadi, kwa sasa hakina ajenda hiyo kutokana na kukaribisha wasio
wasafi.
Alisema akiwa mpambanaji wa vitendo vya ufisadi, ambavyo
vilisababisha kutishiwa kuuawa baada ya kutangaza ‘Orodha ya Mafisadi’
mwaka 2007, sasa anaungana na Dk Magufuli aliyethubutu kusema ataanzisha
mahakama maalumu kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi, jambo
linaloonesha ana dhamira ya kweli kwa kutaka kutimiza hilo kwa vitendo.
“Ukweli Magufuli ametokana na CCM na ana mapungufu kama binadamu,
lakini ukilinganisha kati ya wagombea urais waliopo, yeye ana nafuu na
anaonyesha dhamira ya kupigania serikali,” alisema.
Dk Slaa alisisitiza kuwa wakati huu mgombea urais yeyote anahitaji
kuwa na wabunge wengi, lakini Magufuli anaonesha dhamira ya wazi kukataa
ufisadi kwa kukataa kuwanadi wagombea ubunge wa chama chake,
wanaotuhumiwa kwa vitendo hivyo.
Alisema, akiwa Chadema mwaka 2010 walimlaumu Rais Jakaya Kikwete kwa
kuwanyanyua mkono wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi, lakini
mwaka huu, Dk Magufuli amekataa kufanya hivyo licha ya kuwa ni wagombea
kutoka chama chake.
Akizungumzia vitendo vya rushwa na ufisadi, alisema rushwa ndogo
zinaathiri wananchi kwa kuwafanya waishi kwa unyonge kuliko kubwa ambazo
madhara kwa wananchi wa kawaida ni kidogo. Alisema anasikitika chama
chake kilichopata umaarufu kwa ajenda ya rushwa na ufisadi na kusikiliza
nyimbo za hamasa kupinga masuala hayo, sasa hawasikiki tena.
“Kwa sasa chama cha ACT ndiyo kimerithi vita ya rushwa na ufisadi na kubeba ajenda kila wanapopita,” alisema.
Alisema Magufuli ameonesha kwa matendo kuwa anayozungumza yanatoka
moyoni na siyo mdomoni, kutokana na kutokuogopa kukosa kura za baadhi ya
watendaji wanaotuhumiwa kuwa mafisadi.
“Kama anatekeleza leo hajapewa rungu na akipewa itakuwaje, kwani
haogopi kupoteza kura kwani ufisadi upo kuanzia vijijini na vitongojini,
hatua hiyo ni ujasiri wa ajabu sana kwa mgombea,” alisema.
Alibainisha kuwa kampeni siyo ushabiki wala shamrashamra, bali ni
kuangalia viongozi bora kwa kuzingatia sera. Alisema yeye baada ya
kusikiliza mikutano na kuangalia kwenye mitandao na kuzingatia mapambano
dhidi ya ufisadi, amebaini hakuna mgombea atakayepambana na ufisadi
kama Magufuli.
Akizungumzia suala la wagombea wawili wa vyama vya CCM na Chadema
kuwa na nafasi kubwa ya kupata ushindi, Slaa alisema kuna michakato
inaendelea wakati huu wa kampeni, ikiwemo kupeleka watu katika mikutano
na kutoa fedha.
Alisema hali hiyo imefanya iwe vigumu kupima ni nani anakubalika zaidi.
Alisema wapo wananchi wa aina tatu, kwamba wapo wanamjua wanayekwenda
kumpigia kura, wengine wanafanya maamuzi kabla ya kampeni na wapo pia
wanaofanya maamuzi kwa kubadilika pole pole mpaka mwisho wa kampeni.
Slaa pia alitahadharisha Watanzania kuwa Tanzania ni mama yao, ambaye
hawezi kutokea mwingine, hivyo akichezewa, watu wote wataathirika na
hawataweza kupata mwingine kama huyo.
Alitaka zifanyike kampeni zinazozingatia amani, kama zilivyofanyika
mwaka 2010. Alisema ikiwa itatokea migogoro, hata wanaotangaza uongozi
hawawezi kutawala makaburi, hivyo ni vyema kuzingatia misingi ya amani.
Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuzingatia sheria katika
kusimamia uchaguzi na kuepuka kuwa sababu ya vurugu. Slaa alisema kamwe
Watanzania wasikubali masuala ya kwenda Ikulu, kuleta balaa nchini bali
kwa ujumla kuzingatia masuala ya kitaifa.
Sign up here with your email