SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemtaka kocha wa muda wa timu ya
taifa Taifa Stars Charles Mkwasa kufanya maamuzi kama atabaki kuwa
kwenye timu hiyo ama Yanga. TFF ilimpa Mkwasa nafasi ya kuwa kocha wa
muda wa Stars baada ya kumfuta kazi Mart Nooij Julai mwaka huu.
Mkwasa pia ni kocha msaidizi wa Yanga. Katika kuiongoza Stars Mkwasa
anasaidiwa na Hemed Morocco wa Zanzibar huku Abdallah Kibadeni akiwa
mshauri wa ufundi. Habari za uhakika zilizopatikana jana kutoka TFF
zilisema Shirikisho hilo limemtaka Mkwasa kufanya maamuzi kwani hakuna
kocha anayeweza kufundisha klabu na timu ya taifa kwa wakati mmoja.
"Maamuzi yameshafanywa kwamba Mkwasa inabidi aamue, kubaki Stars au
Yanga, atapelekewa taarifa rasmi," alisema mtoa habari wetu. Habari
zaidi zinasema, suala la Mkwasa kuendelea kufundisha Yanga ndio sababu
ya mkataba wake kuchelewa.
"Mwanzo kamati ya utendaji ya TFF iliamua kumpa mkataba wa muda
mrefu, lakini suala likaja kwa mwajiri wake Yanga itakuwaje, mpango huo
ukasitishwa, sasa anatakiwa kufanya uamuzi," alisema mtoa habari wetu.Uamuzi huo wa TFF umekuja siku moja baada ya baadhi ya wadau wa soka
kuhoji kocha huyo kuendelea kupiga deiwaka Stars huku akiwa mwajiriwa wa
Yanga. Miongoni mwa waliohoji suala hilo ni Ofisa Habari wa Simba, Haji
Manara ambaye amemwandikia barua ya wazi Rais wa TFF Jamal Malinzi na
kuisambaza kwenye blog mbalimbali na mitandao ya kijamii.
"Yanga ndiyo yenye mkataba na 'master' (Mkwasa) vipi mtu mwenye
mkataba naye kila uchwao yupo na timu ya taifa? Haki ipi hapa yanga
wanaipata?… Lakini mh rais huyo kocha anaweza kujigawa vipi wakati Ligi
Kuu inaendelea? je akae kwenye benchi la ufundi la Yanga au akaangalie
wachezaji wa timu nyingine?… "Nimetafiti vya kutosha kwenye hili, kocha Boniface (Mkwasa) hajawahi
kuhudhuria mechi yoyote ya Simba baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa timu
ya taifa zaidi ya mechi baina ya Simba na Yanga ambayo yeye ni kocha
msaidizi, simaanishi kuwa hapendi kuangalia Simba ila muingiliano wa
majukumu unambana…
"Na kwa hili nina hakika mechi nyingi za Ligi Kuu za timu nyingine
kocha Mkwasa ameshindwa kuhudhuria na kuona wachezaji wengine zaidi ya
mechi zinazohusisha timu yake," aliandika Manara kwenye sehemu ya barua
yake ya wazi kwa Rais Malinzi.
Mkwasa ambaye kwa sasa yupo na Stars kwa maandalizi ya mechi ya
kufuzu michuano ya kombe la dunia dhidi ya Malawi katikati ya wiki
ijayo, hakuwa tayari kulizungumzia hilo akisema hajapata taarifa rasmi
na kwamba atafanya maamuzi baada ya kuzipata. "Sijapata taarifa kutoka TFF kwa hiyo siwezi kuzungumzia hilo,
nitakapopata taarifa, nitajua nini nifanye na nitatoa maamuzi," alisema.
Hata hivyo habari za uhakika kutoka kwa watu wa karibu na Mkwasa
zinasema kocha huyo yupo tayari kuachia Yanga na kubaki na Stars kwa
vile kuwa na kazi mbili kwa wakati mmoja kunamchosha.
"Mwenyewe anasema anachoka kuhudumia timu zote mbili, nadhani
ataondoka Yanga na kubaki Stars kwa kuzingatia uzalendo pia na mapenzi
kwa nchi yake," alisema. Mwisho.
Chanzo: Habari leo
Sign up here with your email