TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezindua kituo cha mawasiliano
kusaidia wadau wa uchaguzi hasa wananchi na wapigakura kupata elimu ya
mpigakura, kuuliza maswali kuhusu uchaguzi, pamoja na kulinda usalama.
Kwa kutumia kituo hicho kilichoko katika jengo la ofisi za NEC jijini
Dar es Salaam, wapigakura watatumia namba ya simu 0800782100 kupiga
bure na kuuliza maswali kuhusu uchaguzi mkuu, ikiwa ni pamoja na kutoa
taarifa za kiusalama.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima alisema hayo jana
wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichofadhiliwa na Shirika la Umoja
wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP).
Alisema tangu Oktoba 12 hadi 18 mwaka huu, kituo kilianza kufanya
kazi kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni na kilimepokea maswali 444
na kutolewa ufafanuzi. Alisema kwa siku ya Jumanne pekee walipokea
maswali 937 yanayohusu mwenendo wa uchaguzi, jinsi ya kupiga kura,
kupotea kitambulisho na masuala mengine.
Alisema kuanzia Oktoba 19 hadi 30 mwaka huu, ndipo kituo kitafungwa kufanya kazi saa 24. Alisema wapo watendaji wa kutosha waliopata mafunzo maalumu kwa ajili ya kujibu na kutoa ufafanuzi wa masuala yote ya uchaguzi.
Kailima alisihi Watanzania kutotumia vibaya kituo hicho kwa kutoa
lugha ya matusi au kufanya wengine kukosa mawasiliano, kwani wana mfumo
maalumu kurekodi simu zote zinazotumika, zinazoingia au kufanya jambo
lolote kinyume na kama lugha za matusi na kushtakiwa.
Akizungumzia upigaji kura, Kailima alisema kisheria hakuna mtu
anayeweza kupiga kura katika kituo ambacho hakujiandikishia na kuwataka
kutojisumbua kwenda kwani hawataruhusiwa.
Alisema sheria inasema wanaoruhusiwa kupiga kura sehemu yoyote ni
mawakala, wagombea na watumishi wa tume, lakini kwa kujaza fomu maalumu
na ikizingatiwa kama akipigia kata aliyojiandikisha, atapiga kura tatu.
“Lakini kama kata ni tofauti, atapiga ya mbunge na rais na kama jimbo
ni tofauti na alipojiandikisha atapiga ya rais pekee huku wenye taarifa
zenye utata kati ya Daftari la Wapigakura na kwenye kitambulisho nao
watajaza fomu maalumu na kama hauna kadi hutaruhusiwa kupiga kura
popote,” alisema.
Chanzo: Habari leo
Sign up here with your email