MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema
anayeungwa mkono na vyama vya CUF,NCCR-Mageuzi na NLD, Edward Lowassa amesema akiteuliwa kuwa rais ataanzisha benki ya maendeleo kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini.
Akihutubia katika viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam jana,
Lowassa alisema kumekuwepo na ugumu wa kupata mikopo kwa wananchi wa
kipato cha chini na hivyo akiteuliwa kuwa rais, ataanzisha benki
itakayotoa mikopo kwa makundi hayo.“Natambua kuwa wananchi wa kipato cha chini wanapata tabu sana katika
kupata mikopo na wengine hawapati kabisa, mimi mkiniteua kuwa rais wenu
wa awamu ya tano, nitaanzisha benki ya maendeleo itakayowahudumia bila
ubaguzi,” alisema Lowassa.
Lowassa ambaye amekuwa akidai anakerwa na umasikini, ameendelea
kusisitiza azma yake kuwa endapo wananchi watampatia ridhaa ya kuwa
rais, ataondoa umasikini uliokithiri nchini na kumfanya kila Mtanzania
kunufaika na rasilimali za nchi yake.
Aidha, alisema ili aweze kufanikisha malengo aliyojiwekea pamoja na
ilani ya chama chake, atahakikisha elimu inakuwa bure kwani hakuna
maendeleo bila ya kuwepo na watu waliosoma na kuelimika. Lowassa alisema nchi ya Tanzania ina fedha nyingi pamoja na
rasilimali za kutosha hivyo ahadi anazozitoa ana uhakika wa kuzitekeleza
kwa kutumia fedha za ndani na sio kutegemea misaada ya wahisani.
Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Temeke kupitia CUF, Abdallah Mtolea
alisema endapo atateuliwa kuwa mbunge wa Temeke, atahakikisha jimbo hilo
linakuwa na maendeleo stahiki kulingana na rasilimali zilizopo katika
jimbo hilo.
Mtolea alisema ataboresha huduma za afya, elimu pamoja na maji ili
wananchi wanufaike na matunda ya uongozi bora ndani ya nchi yao. Katika
ziara zake za kutafuta uungwaji mkono na wananchi, Lowassa jana alifanya
mikutano yake jijini Dar es Salaam katika maeneo ya Mwembeyanga
(Temeke), Segerea (Ilala), Sinza katika Jimbo la Ubungo na Jimbo la Kawe
katika Manispaa ya Kinondoni.
Sign up here with your email
