WIKI mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani
nchini, waangalizi kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Umoja wa Nchi za Ulaya
(EU), wametuma maombi ya kushiriki katika uchaguzi huo na kukubaliwa.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Yahaya Simba alisema mpaka sasa nchi
zilizotuma maombi ya kufanya uangalizi katika uchaguzi huo ni nyingi na
takribani zote zimekubaliwa.
Alitaja nchi hizo kuwa ni pamoja na nchi zote zilizo chini ya Umoja
wa nchi za Ulaya (EU) ambapo pia ndani ya nchi hizo, nchi kama Uingereza
na Finland pamoja na kutuma waangalizi kupitia EU pia zitatuma
waangalizi wake binafsi kama nchi.
Aidha, alisema pia Umoja wa nchi za Maziwa Makuu nazo zimetuma maombi ya kuleta waangalizi wake.
Kwa upande wa Umoja wa nchi za Afrika zitatuma waangalizi wake
watakaoongozwa na Ofisa wa ngazi ya juu ambaye ni aliyekuwa Rais wa
Msumbiji, Armando Guebuza wakati kwa upande wa nchi za Jumuiya ya madola
timu yao ya waangalizi itaongozwa na aliyekuwa Rais wa Nigeria,
Goodluck Jonathan.
“Kwa wenzetu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC), wao watatuma timu kubwa ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya nchi
zote za SADC kuwa ni lazima kusimamia kila uchaguzi,” alisema Simba.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za SADC huanza kutuma timu ya
waangalizi wake katika nchi inayofanya uchaguzi tangu nchi hiyo ikiwa
katika mchakato wa awali wa uchaguzi na siku yenyewe ya uchaguzi.
Alisema nchi zote zinazoomba kufanya uangalizi wa uchaguzi kwa mujibu
wa taratibu hutuma maombi yao kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na hadi sasa hakuna nchi iliyotuma
maombi ya kufanya uangalizi iliyowekewa pingamizi.
Sign up here with your email