TUME ya Taifa ya uchaguzi imesema itatoa ufafanuzi kuhusu
kinachodaiwa kuwa ni mashine za BVR zilizokamatwa jana kwa ushirikiano
wa jeshi la polisi na Maofisa wa Chadema huku chama hicho kikisema
wataalamu wake bado wanazichunguza wakishirikiana na polisi ili
kujiridhisha.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Mstaafu
Damian Lubuva ameliambia MwanaHalisi Online kuwa tume bado inafuatilia
na itatoa taarifa ingawa kwa hatua za awali wataalamu wa tume wamesema
kuwa mashine hizo si sawa na zile za tume ya uchaguzi ingawa zinafanana.
“Bado tunachunguza tuweze kutoa taarifa kamili, lakini tunawasihi
wadau wetu wote watulie waache kuingiza hofu kwani zinawachanganya
wananchi.
“Vile vifaa ni kweli vinafanana na vyetu lakini huyo mtu yeye alikuwa
na mashine zake kusajili wafanyakazi wake, naomba itoshe kwa sasa
waambie wananchi taarifa kamili itatolewa,” amesema Lubuva.
Wakati Lubuva akisema hayo, Wakili kutoka makao makuu ya Chadema,
John Malya amesema wataalamu wake wa IT wapo bega kwa bega na polisi
kujiridhisha iwapo hizo mashine hazihusiani na zoezi la kujiandikisha
lililofanywa na tume ya taifa ya uchaguzi.
Leo mmoja ya vyombo vya habari nchini (sio MwanaHalisi) liliripoti
suala la kutanda hofu katika kiwanda cha MM Steel cha jijini Dar es
Salaam chenye mashine za kusajili majina ya watu kwa mfumo wa
kieletroniki.
Vifaa hivyo ni pamoja na scanner, computer na kifaa cha kuchukua
alama za vidole, ambavyo Mejena wa Mawasiliano wa kampuni hiyo,
Abubakari Mlawa amesema wameamua kuandikisha wafanyakazi wake kutokana
na kukithiri kwa vitendo vya wizi katika viwanda saba walivyonavyo na
kushindwa kuwatambua wafanyakazi.
Maafisa wa NEC walioripotiwa kuwa eneo la tukio walikiri kuwa mashine hizo zinafanana na zile tume.
“Tulichokiona ni baadhi ya vifaa ambavyo vinafanana na vifaa vya
tume, lakini hatuwezi kuhakikisha kama ni vyetu au sio, tulichokubaliana
na polisi ni kuchukua vifaa hivyo vifanyiwe uchunguzi zaidi ili
tujiridhishe na vifaa tulivyonavyo,” amesema Kaimu Mkurugenzi wa Idara
ya Sera na Mipango wa NEC, Salvisius Mkwera.
Chanzo: Mwanahalisi Online
Sign up here with your email