MWANDISHI wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kukuza
Utawala Bora na Uwazi, Edwin Soko anatarajia kuipandisha kizimbani
serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Soko amewaambia waandishi wa habari kuwa ana nia ya kuifikisha serikali mahakamani chini ya kifungu cha. 6(2) Sheria ya mwenendeo wa makosa sura ya 5 ya sheria za Tanzania juzuu la 2002 , kikisomeka pamoja na kifungu cha. 3,6(b)c.
Serikali inatuhumiwa tuhuma za kutunga kanuni ndogo za utangazaji
kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, huku ikijua kuwa inakiuka
ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nimewaita hapa kwa ajili ya kuwaambia kuwa, ninafungua kesi ya
kikatiba dhidi ya serikali kufuatia kuwepo kwa baadhi ya vifungu ndani
ya kanuni ndogo za maudhui ya utangazaji 2015, zinazokiuka katiba ya
nchi na kuminya uhuru wa mtu na chombo kupata taarifa na kuzisambaza kwa
mujibu wa katiba,” amesema Soko kwenye mkutano huo uliofanyika ofisi za
UPTC jijini Mwanza.
Aliongeza kwamba licha ya kubaki siku chache, kimsingi yeye pamoja na
wanahabari wengine walihitaji muda wa kujiridhisha kwa kina juu ya
uwepo wa vifungu ndani ya kanuni vinavyokiuka haki ya kikatiba kama
ilivyoainishwa kwenye ibara ya 18, kazi hiyo ilihitaji muda wa kutosha
ili kufanya uchambuzi wa kina na kubaini mapungufu.
Alibainisha baadhi ya vifungu hivyo kuwa ni kanuni ndogo za maudhui
ya utangazaji 2015, vinavyokiuka katiba ya nchi baadhi ya vifungu hivyo
ni 15(2),6(a) (7) (a) na (b), 8(2), 10 (10)(a), 9(2), (3) sanjali na
utangulizi wa sehemu ya tatu ya sheria unaosema hakuna kutangaza siku ya
upigaji wa kura, huku kwenye maudhui ya sheria hii inaruhusu matangazo.
Kanuni hizo zilizotangazwa kwenye gazeti la serikali Juni 26, 2015
zinaminya uhuru wa mtu kupata na kutoa taarifa kwa mwananchi na pia haki
ya vyombo vya habari vya luninga na redio kupata na kusambaza taarifa,
kwani vinawekewa vizingiti visivyokuwa na lazima kisheria.
Athari za kanuni hizo kwa mujibu wa maelezo ya Soko, kuwa wananchi
wanapokonywa nguvu ya kikatiba waliyopewa katika ibara ya 18(a),(b),(c)
na (d) kwa kutotakiwa kushiriki kwenye programu na pia vyombo vya habari
vinanyimwa fursa ya kutafuta na kufikisha taarifa mbalimbali za
mwenendo wa uchaguzi kwa wananchi kwa kuwekewa mipaka ya kuripoti wakati
wa kampeni na siku ya kupiga kura.
Athari nyingine ni kuwa wamiliki wa vyombo vya habari pamoja na
wanahabari hawapo salama kwa mujibu wa kanuni hizi zenye uwezo wa
kuwashughulikia na matokeo yake yakaonekana kwa wananchi kukosa taarifa
muhimu.
Soko ameithibitishia MwanaHalisi Online kuwa hatua za awali za
ufunguaji wa kesi, ikiwa mosi ni kutoa notisi kwa serikali, hatua hiyo
tayari imefanywa na notisi zimesambazwa kwa Mwanasheria Mkuu wa
serikali, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, na Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Sign up here with your email