Kocha wa Yanga aeleza juu ya matokeo mazuri ya timu yake

Wachezaji wa Yanga wakishangilia



KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amesema siri kubwa ya kikosi chake kufanikiwa kuvunja mwiko wa kuifunga Mtibwa Sugar ilitokana na wachezaji wake kucheza kwa nidhamu ya kiufundi.

Yanga iliondoka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro juzi ikiwa ni ushindi wake wa kwanza uwanjani hapo tangu mwaka 2009.

Katika misimu iliyopita, Mtibwa Sugar wamekuwa wakionesha ubabe kwa Yanga na kuwafunga, lakini mambo yamekuwa tofauti msimu huu ambapo Yanga ilidhamiria kushinda na ikawa hivyo.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao, Pluijm alisema amefurahishwa na kikosi chake kilicheza vizuri kwenye uwanja huo ambao alikuwa akiuhofia kutokana na ubovu tofauti na alivyotegemea.

“Mchezo ulikuwa mzuri tofauti na nilivyotegemea kutokana na uwanja jinsi ulivyo, wachezaji walicheza vizuri na kwa nidhamu ya hali ya juu,” alisema kocha huyo Mholanzi. Alisema jambo lingine lililomfurahisha ni wachezaji wake kuzingatia maelekezo yake na kuondoka na pointi tatu.

Ushindi huo umeendeleza rekodi ya Yanga ambapo tangu wameanza msimu hawajapoteza mchezo hata mmoja wakiendelea kushika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa pointi 15 sawa na Azam FC wakitofautiana katika mabao ya kufunga na kufungwa.

Baada ya mchezo huo, Yanga, Azam FC na Simba hawatakuwa na michezo ijayo ya ligi kwa ajili ya kuwapa nafasi wachezaji walioteuliwa kwenye timu ya Taifa kujiunga na kambi ya maandalizi ya mechi dhidi ya Malawi.

Kulingana na ratiba ya TFF, kesho Yanga ilikuwa icheze na African Sports kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam na Ndanda FC dhidi ya Simba mjini Mtwara, lakini mechi hizo zimeoneshwa zitapangiwa tarehe nyingine.

Ratiba inaonesha timu zitakazocheza kesho ni Mgambo JKT dhidi ya Coastal Union jijini Tanga, Majimaji itaialika Mwadui FC, Toto Africans itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu wakati keshokutwa Stand United itacheza dhidi ya Mbeya City na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons.

Baada ya mechi ya timu ya Taifa, Oktoba 17, mwaka huu, Yanga watacheza na Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Simba dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Previous
Next Post »
Show Comments: OR

Contact us

Name

Email *

Message *

Tangaza nasi

Tangaza nasi
Freebango.com