Polisi mkoani Pwani, imeweka bayana sababu za kitaalamu za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila ikisema alivunjika mbavu nane upande wa kushoto, damu kuingia kwenye mfumo wa hewa na kushindwa kupumua.
Mchungaji Mtikila alifariki dunia juzi alfajiri baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Njombe kwenda Dar es Salaam, likiwa katika mwendo mkali, kuacha njia na kupinduka. Alirushwa nje kupitia kioo cha mbele kutokana na kutofunga mkanda.
Katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Msolwa, Chalinze mkoani Pwani, watu wengine wawili waliokuwa kwenye gari hilo dogo walijeruhiwa na dereva anashikiliwa na polisi akitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed alisema jana kuwa baada ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, madaktari katika hospitali Teule ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi walibaini kuwa sababu hizo ndizo zilizosababisha kifo chake.
Wapata ajari wakiwa Njombe:
Pia imegundulika kuwa, kabla ya ajali hiyo kutokea, Mtikila na abiria wenzake ambao waliondoka Dar es Salaam Oktoba 2 jioni kwenda Njombe na kufika Oktoba 3 alfajiri kwa ajili ya kampeni za chama chake, wakiwa huko walipata ajali kwa kugonga magari mawili yaliyokuwa pia yamepata ajali na kusababisha uharibifu wa gari lao hilo.
“Kulingana na taarifa ya mkaguzi wa magari ya Oktoba 3, huko Njombe, walishauriwa watengeneze gari lao kwanza kabla ya kulitumia tena. Saa 3.30 usiku waliondoka Njombe kurudi Dar es Salaam na ilipofika saa 11.45 alfajiri Oktoba 4 ndipo wakapata ajali,” alisema Kamanda Mohamed.
Uchunguzi wa Poilisi:
Alisema uchunguzi uliofanywa kwa kukagua tukio zima la ajali na kuwahoji majeruhi, umeonyesha kuwa ajali hizo zimesababishwa na mambo manne.
Kamanda Mohamed aliyataja mambo hayo kuwa ni ubovu wa gari kwa kuwa lilipopata ajali Oktoba 3, moja ya sehemu muhimu ziliyoharibika ni mfumo wa usukani, hivyo inawezekana halikupata matengenezo kikamilifu na hivyo kuchangia ajali hiyo ya pili.
Jingine ni Mtikila kutofunga mkanda wa usalama na hivyo kusababisha arushwe nje kupitia kioo cha mbele, uchovu wa dereva kutokana na safari ndefu ya kuendesha gari mchana na usiku na kabla ya safari kurudi alikuwa akishughulikia matengenezo ya gari hivyo hakupata muda wa kupumzika.
Sign up here with your email